Ikimbize Siku, Usiiache Ikukimbize


Categories :


Moja ya vitu vinavyolalamikiwa na watu wengi ni ufinyu wa muda. Limekuwa lalamiko la watu kuwa muda hautoshi. Kila unayemuuliza kwa nini hafanyi kitu fulani, atakwambia hana muda. Kwa mfano kwa nini watu wengi hawasomi vitabu vya kuongeza maarifa ya maisha yao binafsi au kuhusu kazi zao, watakuambia hawana muda.

Kitu kizuri ni kuwa kuna usawa katika mgao wa muda. Kila mtu ana masaa ishirini na nne kwenye siku, hakuna hata mmoja aliyeongezewa au kupunguziwa hata sekunde moja. Hii ni sababu ya wazi kabisa kuwa kama kuna mtu mnafanana umri na yeye amepiga hatua kubwa zaidi tambua kuwa sababu yake itakuwa ni utofauti kwenye matumizi sahihi ya muda.

Matumizi ya siku unayoachiwa uiishi ndiyo yanayoamua nini unakipata katika maisha yako. Watu wengi wamekuwa wakikimbizwa na siku tangu anapoamka mpaka anapoenda kulala. Anaenda kulala akiwa amechoka, ukimuuliza akuambie nini cha muhimu amekikamilisha, hana. Ili uweze kuitumia siku yako vizuri na kufikia mafanikio makubwa huna budi kuikimbiza siku na sio kukubali kukimbizwa nayo. Unakubali kukimbizwa na siku pale unapokubali muda ukupangue kitu chochote kufanya na si wewe kuthibiti nini ufanye kwa wakati gani. Ikimbize siku yako kwa namna ifuatayo;

Ipangilie siku yako: Kutokujua kwa dhati, kitu gani utafanya na muda gani ni kuchagua kufanya chochote na muda wowote. Huko ndiyo kuchagua kukimbizwa na siku. Kabla ya kulala au asubuhi mapema unapoamka panga jinsi utakavyoiendesha siku yako, ili unapoianza unajua nini unaenda kukifanya. Kutoipangilia siku yako, ni kuchagua kuipoteza.

Weka vipaombele: Kuna jambo au mambo machache ambayo unaona ukiyakamilisha siku hiyo yataleta thamani kubwa sana kwenye malengo yako. Hayo ndiyo mambo ya kuanza nayo. Muda mzuri wa kuanza na hayo mambo ni asubuhi ambapo unakuwa bado una nguvu na utulivu mkubwa. Fanya jitihada za kuhakikisha umeyafanya hayo ndipo utakapoenda kulala ukijiona ni mshindi.

Amka mapema:  Asubuhi ni muda mzuri wa kufanya mambo makubwa. Ukiwahi kuamka kabla ya watu wengi hawajaamka unapata muda tulivu wa kufanya mambo kwa ufanisi mkubwa. Huu ni muda ambao akili inakuwa bado ipo ‘fresh’ na hivyo kukuwezesha kutafakari mambo makubwa kama kusudi, ndoto, malengo na nini unaenda kufanya siku hiyo. Lakini pia ni muda mzuri wa kusoma, kusali, kutahajudi, kufanya mazoezi nk. Ukifanikiwa kuamka mapema na kufanya haya, unajihakikishia kuikimbiza siku hiyo kwa ushindi mkubwa.

Weka umakini: Matumizi mazuri ya muda yanahushisha pia uwepo wa akili yako kwenye jambo unalolifanya. Umakini huongeza ubora wa kazi na pia huokoa muda. Watu wamekuwa wakihamisha mawazo kwenye kazi na kumpeleka sehemu nyingine. Kwa kufanya hivyo wanapata vitu nusu nusu. Hakikisha akili yako inakuwa kwenye kile unachokifanya ili akili yako ikimbie na muda badala ya akili yako kuruka ruka huku na kule.

Kuwa na nidhamu: Utafanikiwa kuuendesha muda wako kama utakuwa unafanya yale uliyoyapanga kwa wakati uliopanga. Watu wengi wanapanga vizuri nini wafanye lakini hawafanyi walivyopanga. Ili uweze kuikimbiza siku hakikisha unajisukuma kufanya kama ulivyopanga. Hii inahusisha kufanya kwa sababu inakubidi ufanye na si kwa sababu unajisikia.

Gawa majukumu: Huwezi kufanya kila kitu mwenyewe. Ili uweze kuitumia siku vizuri wagawie watu wengine wanaoweza kufanya majukumu uliyoyapanga kwa ustadi mkubwa. Utafanikiwa kukimbiza siku yako kwani mwisho wa siku utakamilisha mambo mengi kuliko ungeamua kufanya kila kitu mwenyewe.

Fanya tathmini: Huwezi kujua kama umeitumia siku vizuri bila kujitathmini. Kabla hujalala jiulize umeitumiaje siku yako. Umetimiza kwa kiasi gani yale uliyoyapanga? Hii itakupa nafasi ya kuboresha maeneo ambayo hukuyafanya vizuri leo na kuwa bora zaidi kesho. Huwezi kujua urekebishe wapi kama hujui ni wapi siku iliyopita ilikukimbiza.

Ndugu, mafanikio yako ya miaka mingi ijayo yapo kwenye namna unavyoiishi siku yako. Itakuwa ni vigumu kupiga hatua kubwa kama utakubali kukimbizwa na siku, bali ipangilie siku yako vizuri kuhakikisha unaiendesha siku yako kwa faida kubwa.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *