Mfahamu Leo Anayeweza Kukupa Maisha Bora Uliyoyatamani Kwa Siku Nyingi.
Maisha bora yenye mafanikio makubwa limekuwa tamanio la watu wengi maishani. Kuna maisha fulani ambayo umekuwa ukiyatamani tangu utotoni kwako lakini mpaka leo bado hujayapata. Umekuwa ukiamini kuwa ukiyapata maisha haya, furaha itatawala na maana ya maisha yako hapa duniani itadhihirika.
Umekuwa ukiota kila siku kama maisha hayo yapo sehemu fulani hivi na kuna siku yatakuja. Mara nyingine umetamani muda uende kasi ukifikiri mafanikio hayo yatakuja kwako baada ya muda fulani hata kama huweki kazi yoyote. Mara nyingine umefikiri kuwa serikali ndiyo ambayo itakupa maisha hayo unayoyatamani. Muda mwingine umefikiri ni wazazi wako wanaotakiwa wakupatie maisha hayo. Kadhalika baada ya kuwaona watu wengine wakipata vile walivyovitaka, ukajiambia hao bahati yao imefika na wewe muda wako wa bahati utakuja.
Maisha hayo mazuri ninayotamani yatatoka wapi? Nani atanipa maisha ninayotamani? Lini nitaishi maisha haya ninayotamani? Je sijachelewa kuyapata maisha haya? Haya ni miongoni mwa maswali ambayo umekuwa ukijiuliza kuhusu maisha ya matamanio yako. Kuna mtu mmoja anayeweza kukupatia maisha uliyoyasubiri muda mrefu. Bahati nzuri mtu huyo hayupo mbali sana na wewe. Kingine ambacho ulikuwa hukifahamu ni kuwa mtu huyo umekuwa naye kwa muda mrefu sana. Mtu huyo ni wewe mwenyewe, ndiyo, WEWE MWENYEWE.
Wewe ndiye mtu sahihi kabisa wa kutengeneza maisha uliyoyasubiri kwa muda mrefu. Kwa sababu wewe upo hapo ulipo, una nafasi ya kuanza kuyatengeneza maisha hayo hata leo. Uzuri ni kuwa una kila zana ya kutengeneza maisha hayo. Kuanza kutengeneza maisha hayo anza kufanya yafutayo;
1.Tambua kwa wazi kabisa nini hasa unakitaka maishani mwako. Kila mtu ana kitu kinachomsukuma toka ndani mwake akiamini akikifanya au kukipata hicho moyo wake utaridhika. Kaa chini na tafakari ni kitu gani hicho? Kisha kiweke kwenye maandishi kwa kukiandika kwa mkono wako mwenyewe. Je unataka kuwa na biashara kubwa itakayokidhi mahitaji wa watu? Je unataka uhuru wa kifedha?
2. Weka mipango. Kujua tu unachokitaka bila kuweka malengo kisha mipango ya kufikia unachokitaka ni bure. Bila kuweka kazi tena kubwa hutakipata kile unachotaka. Weka malengo na mipango kisha anza kuchukua hatua za kupata kile unachokitaka.
3. Anza na ulicho nacho. Matokeo unayoyatamani yanaweza kuwa makubwa sana kiasi cha kuhisi huwezi kuyafikia ukiangalia nini ulichonacho mkononi. Unajiuliza utaanzia wapi? Kwenye kila kitu kuna sehemu ya kuanzia kabla hujapata kile kikubwa. Ulichonacho mkononi mwako ndiyo cha kuanzia. Weka akiba kwenye kila kipato unachokiona ni kidogo, lakini ukikiweka kwa muda mrefu kitakuwa kikubwa na kupata mtaji wa kuanza biashara ya ndoto yako.
4. Kimbia badala ya kutembea. Umepoteza muda mwingi kwa kusubiri mtu atakayetengeneza maisha unayoyataka. Baada ya kujua ni wewe wa kutengeneza maisha ya ndoto yako, huna muda wa kupoteza tena. Inakupasa kukimbia wakati wengine wanatembea. Weka kazi kubwa na nidhamu ya hali ya juu kwenye kila unachopanga.
5. Maarifa zaidi. Kuna watu ambao walianza kuchukua jukumu la kuishi maisha yao kabla yako. Walianguka kwa kufanya makosa, lakini waliinuka, kujifunza kisha kuendelea na safari. Hawa watu wana maarifa ambayo ni msaada kwako kwenye safari ya kutengeneza maisha yako. Soma na sikiliza vitabu na maarifa yao mengine ili wewe usirudie makosa hayo sasa. Pia maarifa haya yatakuwa mwongozo mkuu wa wewe kupiga hatua kubwa.
Ndugu umesubiri maisha ya ndoto yako kwa muda mrefu sasa. Umeshampata mtu wa kukupatia maisha hayo. Weka wazi kabisa kwenye maandishi nini unataka. Ili kuhakikisha unaanza kutengeneza maisha ya ndoto yako kwa usahihi, nimekuandalia mwongozo wa kuweka na kutimiza malengo yako. Huu mwongozo utakusaidia kuweka malengo yenye sifa bora, kuwagawa malengo kwenye vipande, kuyaishi, kuyatathmini kisha kupata matokeo ya kile unachokitaka. Mwongozo huu unaupata bure kabisa kwa kubonyeza kiunganishi hiki ili kuupakua https://www.amshauwezo.co.tz/mwongozowamalengo
Pia uwezo wa kupata maisha unayotaka upo ndani yako, kinachotakiwa ni kuuamsha tu uwezo huo na kuanza kuutumia. Ili kuutambua uwezo mkubwa ulionao tangu kuzaliwa na kuuamsha, pata kitabu cha AMSHA UWEZO WAKO HALISI kwa kupiga simu namba 0752 206 899.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
