Dawa Ya Nne Ya Kutibu Ugonjwa Wako Wa Kushindwa.


Categories :

Hongera kwa kupata dawa tatu za awali kwa ajili ya kutibu ugonjwa wako wa wa kushindwa. Kama tulivyokubaliana kuwa ungonjwa huu unahitaji muunganiko wa dawa nyingi
ili kuweza kupona.

Baada ya kupokea dawa ya kwanza ya kutibu mtazamo wako, dawa ya pili ya kukuponya kufanya vitu bila ya kuweka malengo, pia dawa ya kutibu kutokuweka kazi na badala yake kujenga urafiki na kazi, dawa ya inayofuata ni ya kutibu kuto kutekeleza uliyopanga, dawa hiyo ni nidhamu.

Nidhamu ni kufanya kile ulichopanga bila kusikiliza sababu yoyote ile. Kazi huenda sambamba na nidhamu. Ili uweze kufanya kazi na kupata matokeo ya kutimiza malengo yako, huna budi kuwa na nidhamu.

Nidhamu inahusisha kufanya vitu hata kama hujisikii kufanya. Huku ndiko kumekuwa na changamoto nyingi. Watu wanapenda kufanya kazi pale tu wanapojisikia; kwa sababu miili yetu ina asali ya uvivu, kufanya kazi kwa kujisikia ndiko kuwesababishia watu wengi kuugua ugonjwa huu wa kushindwa. Kuna aina nyingi za nidhamu, lakini tutagusia aina nne ambazo unatakiwa uzijenge ili kupona ugonjwa wako wa kushindwa;

Nidhamu binafsi: Hi ni nidhamu inayokuhusu wewe binafsi jinsi unavyoitikia kwenye matukio mbalimbali. Kwa mfano umepanga kutoshiriki kwenye mabishano yasiyo na maana, je mabishano hayo yakianza unafuata kile ulichopanga? Umepanga kutokuhofia kuchukua hatua za misingi wa mafanikio yako, je ukifika muda wa kuchukua hatua, huhofii? Ukijenga nidhamu hii itakuwa rahisi kujenga nidhamu nyingine. Fanya yale uliyopanga kufanya kwa ajili yako.

Nidhamu ya muda: Hapa ndipo pana changamoto kubwa pia. Sababu kubwa ya kuchelewa kupata matokeo na kuishia kuwa na maisha ya kawaida ni kwa kwa sababu ya kukosa nidhamu muda. Muda ukipotea huwezi kuupata tena. Waliofanikiwa wanatumia muda wao vizuri. Wanapanga nini cha kufanya kwenye kila dakika ya siku na kuhakikisha wanakifanya hicho. Usikubali muda wako upotee bila ya kufanya kitu chochote cha maana.

Nidhamu ya fedha: Je fedha yako unaitumia kama ulivyopanga? Ni mara ngapi umetumia fedha uliyosema ya akiba kwenye kununua kitu ambacho hakikuwa kwenye bajeti yako? Je huoni hili ndilo liliokusababishia wewe kukosa fedha ya mtaji mpaka leo. Kwenye kila kipato unachotegemea, gawanya kabisa matumizi yake hata kabla hujaipata, kisha tumia kama ulivyogawanya baada ya kupata fedha hiyo.

Nidhamu ya kazi: Kazi ni msingi wa mafaniko yoyote, bila kazi hakuna matokeo na kama hakuna matokeo hakuna mafanikio. Kama tulivyoona kwenye makala ya jana kuwa ili uweze kufanikiwa kwenye maisha yako, huna budi kujenga urafiki na kazi.

Kukosa nidhamu kunapelekea kuahirisha mambo. Sababu kubwa ya kuahairisha na baadaye kufuta kabisa kitu unachotaka kukifanya ni kukosa nidhamu yaani kutokufanya kama ulivyopanga au kufanya pale tu unapojisikia. Ndiyo maana ni muhimu sana kupata dawa hii ya kutibu kukosa nidhamu ili uweze kupona kushindwa kwako.

Njia mojawapo kuu ya kujenga nidhamu ni kuwa na shauku kubwa ya kile unachokifanya. Ili uwe na shauku kubwa ni lazima uwe na KWA NINI KUBWA ya kile unachokifanya. Kuna maumivu makali ya kujenga nidhamu kali ya kufanya na tena kwa msimamo hivyo unahitaji kutambua sababu ya kwa nini ujitese? Je ni kwa sababu ya umasikini ambao unakukumba wewe na jamii yako hivyo unataka kuwa mkombozi? Tambua kusudi lako na jenga ndoto yako kubwa; hivi vitakusaidia kutambua kwa nini kubwa ya kujenga nidhamu kali katika maisha yako.

Kuanzia leo hakikisha unafanya kila ulichopanga kukifanya. Usisubiri mpaka ujisikie, wewe fanya mradi tu hicho ndicho kinachotakiwa kifanyike.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *