Hivi Ndivyo Umekuwa Ukilisukuma Gari Ukiwa Ndani Ya Gari Hilo Ukitarajia Litatembea.


Categories :



Moja mbili tatu, sukuma! Moja mbili tatu, sukuma! Mbona gari halisogei? Hizi zilkuwa ni sauti za watu waliokuwa wanasukuma gari angali na wao wakiwa wamepanda humo humo. Licha ya idadi yao kuwa kubwa na wakiwa wenye nguvu lakini jitihada zao hazikuweza kuzaa matunda ya kulifanya gari lisogee. Jambo hili liliwafanye washangae sana.

Inawezekana na wewe hujawahi kujiuliza kama unaweza kusukuma gari wakati mwenyewe ukiwa ndani ya gari hilo. Lakini hiki ndicho hawa jamaa kilichowapata, unaweza kufanya majaribio pia. Lakini kwa kujua au kutokujua, ni kitu ambacho umekuwa ukikifanya maishani mwako. Naamini utakuwa umeshangaa sana na kujiuliza ni lini wewe ulikaa ndani ya gari na kuanza kulisukuma!? Lakini ukweli umekuwa ukifanya hivyo.


Umekuwa ukisukuma gari ukiwa ndani na kutarajia litembee kwa kutarajia matokeo fulani mazuri na sahihi angali ukifanya mambo yasiyo sahihi. Kuna hatua nyingi tu umekuwa ukizichukua ambazo haziendani na matokeo unayoyataka lakini umeendelea kujifariji kuwa utayapata matokeo hayo. Unapoteza muda tu ndugu, badilika sasa. Kumbuka kanuni ya kisababishi na matokeo ambayo inaeleza wazi kuwa kwenye kila matokeo yanayotokea kuna kisababishi nyuma yake.

Hivyo kwenye kila matokeo unayoyataka ili yajenge mafanikio katika maisha yako, hakikisha umeweka kisababishi sahihi kinacholingana na matokeo unayoyataka. Hivi ndivyo umekuwa ukisukuma gari ungali umelipanda ukitarajia litembee;

Hutoi thamani lakini unatarajia mafanikio. Umekuwa ukitamani kupata mafanikio na hasa mafanikio ya utajiri lakini umekuwa ukifikiri ni muda tu ndio utakupa utajiri huo bila ya kuwapa watu thamani. Kama kipato cha sasa hakijakufikisha utajiri na hakuna mipango yoyote ya kuongeza thamani, kutarajia kupata utajiri katika mazingira hayo, ni wewe kujaribu kulisukuka gari hilo ungali upo ndani ya gari hilo. Fikiri kwanza namna kuongeza thamani, ndipo unapoweza kupata utajiri.

Unakaribisha mawazo hasi ukitarajia uwe na furaha. Chanzo cha furaha katika maisha yako ni mawazo unayoyaruhusu yaingie ndani yako na kuyaacha yazame ndani yako. Mawazo ya hasi ni kama vile chuki, wivu, dharau nk hivi vyote vitakupelekea kwenye huzuni. Ili uweze kuwa na furaha ya kudumu maishani mwako hakikisha unaruhusu mawazo chanya kila wakati. Mawazo chanya ni kama upendo, shukrani, imani, ukarimu. Kutegemea kupata furaha ungali unamiliki mawazo hasi ni sawa na kusukuma gari ungali upo ndani gari hilo.

Kuahirisha mambo huku ukitarajia matokeo. Kuna wakati umekuwa tayari ina mipango mizuri ya kufanyia kazi ili uweze kupata matokeo. Lakini muda ukifika wa kutekeleza mipango hiyo umeahirisha na kusema kesho na kesho ilipofika ukaiona kesho nyingine, hivyo hukufanya ukasema kesho tena. Baada ya kujua kitu sahihi cha kufanya ili kupata, bila kujali sababu yoyote ile hakikisha umefanya na kuvumilia mpaka kupata matokeo. Vinginevyo ni sawa na wewe kusukuma gari ukiwa ndani ya hilo gari ukitegemea litatembea.

Kutopangilia muda wako ukidhani utatimiza vipaombele.
Duniani kuna mambo mengi ambayo utatamani uyafanye. Hata pale unapokuwa hujajipa majukumu hayo, dunia inaweza ikakupatia uyafanye. Ndiyo maana unaweza ukakutana na vitu vingi sana unavyotakiwa uvifanye kiasi cha kutokujua uanzie wapi. Hii imekuwa sababu ya watu kufanya jambo lolote kama hawatakuwa makini. Lakini kuna vitu vingi sana ambavyo unaweza ukawa navyo busy lakini vikawa na mchango mdogo sana kwenye mafanikio yako. Hivyo unahitaji kuwa na vipaombele katika maisha yako; unapoamka asubuhi tambua nini kipaombele chako katika siku hiyo. Kuendelea kufanya lolote bila kuwa kuweka vipaombele ni kusuka gari ungali umepanda ndani yake.

Unataka kupata nini maishani mwako; je ni utajiri? Furaha? Amani? Umaarufu? Afya njema au mafanikio gani? Unaweza kupata chochote unachotaka, lakini tambua kwanza kitu gani sahihi cha kufanya ili upate unachotaka, fanya hicho kwani hakuna njia ya mkato.


Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi,
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *