Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukaa Kwenye Moto Wa Tanuru Na Kupata Kile Unachokitafuta.
Tofari bichi halina thamani likiachwa hivo hivyo bila kupitishwa kwenye tanuru. Ila likiwekwa kwenye tanuru kisha likavumilia moto mkali uliopo huungua na kuiva kisha kuwa na thamani kubwa.
Thamani ya tofari hilo huongezeka na kuwa kubwa kulingana na ukubwa wa moto. Ndiyo maana zile tofari zitakazokaa karibu na moto na kuuvuilia moto ndizo zitakazoiva vizuri kuliko zile zitakazokaa nje na mbali na moto.

Maisha yako ya mafanikio makubwa yanakuhitaji uive na kuwa na thamani kubwa. Kuna moto wa maisha ambao hutakiwi kuukwepa ili uweze kuiva. Thamani za watu wengi zimepungua baada ya kuukimbia moto huu na hivyo kushindwa kuiva.
Moto wako wa tanuru ni changamoto zinazosimama katikati ya mafanikio yako. Hakuna mafanikio yasiyo na changamoto, kadri unavyo panga kupata mafanikio makubwa ndivyo unavyokutana na changamoto kubwa pia. Changamoto ni vikwazo vinavyosimama katikati ya mipango na mafanikio. Ili kuweza kupata matokeo unayoyataka hunabudi kupita katikati ya tanuru hilo la changamoto. Utafanikiwa kuyapata mafanikio nga’mbo yake kama utakubali kuivishwa na moto ufuatao;
Moto wa kukataliwa. Huwa unajisikaje pale unapokuwa na jambo uliliazisha ukiamini ni zuri na kila mtu atalikubali, halufu mwisho wa siku kila mtu akalipinga? Huwa unapata ujasiri wa kuendelea na biashara ambayo ulifikiri ukifungua tu wateja watajaa lakini siku ukakaa kuanzia asubuhi mpaka jioni bila ya hata mteja mmoja? Huu ndiyo moto unaokuivisha. Ukivumilia katika kukataliwa kwako utafanikiwa kuwa na thamani kubwa.
Moto wa kukatishwa tamaa. Licha ya mipango mizuri unayoipanga, bado vitu huwa havitokei kama unavyotarajia. Kuna kipindi mtokeo yanachelewa kutokea, je huwa unakata tamaa? Iva kwenye moto huu kwa kuendelea kufanya hata pale matokeo yanapochelewa.
Moto wa hisia hasi. Moja ya kitu kinachowafanya watu wayachukie maisha ni hisia hasi. Hizi ni hisia zinazoiba furaha na nguvu za mtu. Kuna mazingira mengi yanayoweza kukusababishia hisia hasi. Kwa mfano watu kukuudhi hata bila sababu. Je katika mazingira kama hayo huwa unaendelea kufurahia maisha? Ivishwa na moto huu ili furaha yako iwe kwa sababu ya uhai wako.
Moto wa hofu. Kufanya vitu vikubwa ambavyo hujawahi kuvifanya kunaleta hofu. Wale wanaouvaa ujasiri na kuviendea vile wanavyotaka kuvifanya ndiyo wanaofanikiwa. Ukitaka kufanya jambo fulani kubwa ukaanza kupata hofu huwa unafanya nini? Je unaogopa na kurudi nyuma?
Moto wa kushindwa. Watu wengi huwa hawaupendi kusikia wimbo kushindwa masikioni mwao. Je unachukuliaje pale unapoweka jitihada katika mpango wako halafu haukupi matokeo? Unaendelea au unaishi hapo? Au unatafuta mchawi?
Waliofanikiwa walipita katika moto huu na kuiva. Lich ya kushindwa mara nyingi waliendelea na vile walivyoviamini mpaka waliaanza kupata matokeo.
Ndugu! Kama unataka uwe thamani kubwa kisha kupata mafanikio makubwa huna budi kuanza kuvumilia moto wa tanuru ili kuiva vizuri. Huku ni kuishinda kila changamoto itakayosimama kabla ya mafanikio yako.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika
Kocha na Mwalimu wa uwezo wako halisi
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
