Hii Ndiyo Dhambi Kubwa Uliyoitendea Chumbani Kwako.
Ukitenda kosa linalohusisha watu wawili, unaweza kujitetea kuwa jirani yako ndiye aliyekushawishi. Lakini unapotenda dhambi ungali upo pekeyako hakuna mtu wa kumsingizia kuwa ndiye aliyesababisha.
Kuna dhambi moja ambayo umekuwa ukiitenda pekeyako tena chumbani kwako. Hii ndiyo iliyokubakisha chumbani kwako mpaka sasa. Kwa sababu hujatoka nje ya chumba chako, watu wameshindwa kukutambua wewe ni nani wala kufaidi kile ulichonacho mikononi mwako.
Natambua utakuwa na hamu kubwa ya kujua ni dhambi gani hiyo umeitenda! Kwa sababu natamani uitambue dhambi hiyo ili uitubu na kupona nami nakuambia leo kuwa dhambi hiyo ni KUJIDHARAU. Hii ni dhambi kubwa sana kwako, umeitenda na imekugharimu sana maishani mwako. Inawezekana umetenda kwa kujua au kutokujua, lakini ndiyo sababu ya kutopiga hatua kabisa au hatua hizo ndogo ulizozipiga.
Kujidharau ni kujidanganya mwenyewe. Kujidharau ni kujiambia wewe huna thamani ndani yako na mbele ya watu mengine. Kwa kufanya hivyo umejiona mnyonge na kuona kuna watu fulani ndiyo waliopendelewa maishani mwako.
Kama simba angejidharau, angejiona yeye ni kama nyani mbele ya tembo na kutokujaribu hata kumgusa. Lakini kwa sababu hajaruhusu kijidharau, huuona uwezo wake wa kumgeuza tembo kitoweo licha ya ukubwa wa tembo alionao.
Hujauona upekee wako kwa sababu ya kujidharau. Licha ya dunia kuwa na watu zaidi ya bilioni 8 lakini yupo WEWE mmoja tu. Ndiyo! Hufanani na mtu mwingine yoyote. Una upekee fulani ndani yako ambapo usipouonyesha dunia haiwezi kuupata kokote. Upekee huo ni wa kufanya vitu vya kipekee kwa kiwango kikubwa cha kipekee na kupata matokeo makubwa ya kipekee. Lakini kwa kujidharau kwako, umeshindwa kuuona upekee huo wala dunia haijaushuhudia. Tubu dhambi hii leo.
Umeishi ndoto ndogo kwa sababu ya kujidharau. Huwezi ukaota kufanya mambo makubwa katika kipindi cha uhai wako kama utajidharau na kujiona wewe huna uwezo wa ndoto kubwa. Ndiyo maana umekuwa ukijewekea mipaka kuwa mimi ni wa kiwango hiki kidogo na mambo haya makubwa ni ya watu fulani. Ndoto kubwa ni haki ya kila mtu. Tubu dhambi hii leo.
Umeishi kwa kuiga kwa sababu ya kujidharau. Usipojiona wa pekee, utajidhara kwa kuona wewe huwezi kubuni kitu chochote. Badala yake umeangalia walichokifanya watu wengine na kisha na wewe kuiga hicho. Wewe sio wa kuiga bali wa kubuni. Tubu dhambi hii leo.
Umeona huwezi kuwa tajiri kwa sababu ya kujidharau. Mimi siwezi kuwa tajiri. Ni kweli kabisa kwa imani uliyonayo huwezi kuwa tajiri. Kitu ambacho akili inakiamini ndicho unachokipata. Umeamini kwenye umasiki, ndiyo ulioupata. Lakini umasikini umekuja baada ya kutenda dhambi hii ya kujidharau. Unaweza kuwa tajiri kwa kuanza kutoa thamani kubwa kwa kutumia upekee wako. Tubu dhambi hii leo.
Umeendelea kuubembeleza uwezo wao kwa sababu ya kujidharau. Una hazina ya nguvu kubwa ndani yako. Nguvu hii uliumbwa nayo, hivyo ipo ndani yako. Hii ni ya kukuwezesha kufanya makubwa. Unaifaidi nguvu hii pale unapoiamusha kwa kuweka malengo makubwa na kuanza kuyatimiza. Lakini umeshindwa kuifaidi kwa kujidharau. Tubu dhambi hii leo.
Ndugu! Dhambi hii unaifanyia chumbani kwako yaani ndani yako. Hii imebebwa na mtazamo ulionao ambao upo ndani yako na hakuna mtu mwingine ndani yako mpaka pale unapomruhusu. Hivyo dhambi hii inatubika chumbani huko huko. Itubu kwa kubadili matazamo wako. Wewe ni wa thamani kubwa sana, hakuna mfano wako, kwa nini kujidharau? Kuna mabadiliko makubwa sana yatatokea baada ya kubadili tu huu mtazamo. Mtazamo wa zamani unapokurudia uukatae uuambie mimi naweza, mimi ni wa thamani kubwa, mimi ni wa pekee na ni tajiri.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
