Muda Unaenda! Badili Wachezaji Ili Upate Matokeo.
Kila timu inayoshiriki mechi ya mpira wa miguu huwa na wachezaji kumi na moja ndani ya uwanja. Lakini pia kila timu huwa na wachezaji kadhaa nje ya uwanja kwa ajili ya kufanyia mabadiliko.
Pale mchezaji mmoja uwanjani anapoumia na kushindwa kuendelea na mchezo, kocha hulazimika kumtoa na kumuingiza mchezaji aliyekuwa nje. Pia kocha huamua kumtoa mchezaji yule ambaye hafanyi vizuri na kumwingiza mchezaji mwingine ambaye anaamini atafanya vizuri zaidi ya yule aliye uwanjani kwa muda huo.
Wewe ndiyo kocha wa mechi yako ya mshindano hapa duniani. Mshindani wako mkuu kwenye mechi yako ya ushindini ni changamoto ambazo huwa hazipo tayari kukuona ukishinda mechi na kupata mafanikio kirahisi. Kama ilivyo kwenye mechi za mpira wa miguu kuwa na muda maalumu wa mchezo ndiyo ilivyo kwako, una muda maalumu japo hujui ni lini utaisha.
Kocha hubadili wachezaji na sio lengo la mechi. Kila mechi huwa na lengo lake, na pale kocha anapoona mchezaji aliyoko ndani anashindwa kutimiza lengo, ndipo humutoa na kumuingiza yule anayefikiri anaweza kutimiza lengo hilo. Mbinu zako za awali za kupata mafanikio zinaposhindwa usibadili lengo bali badili mipango yako ili kulifikia lengo.
Wakati mpira ukiendelea kocha huendelea kufanya tathmini. Ili kujua mwenendo wa timu yake, kocha huendelea kuutazama mchezo na kubainisha uimahiri na udhaifu wa timu yake. Kisha kurekebisha makosa ili kuweza kufanya vizuri zaidi. Hakikisha unaifanyia tathmini mipango yako kwa kubainisha kasoro zilizopo kisha kufanya marekebisho mapema. Je unahitaji maarifa zaidi kwenye kile unachokifanya?
Hata timu ikifungwa huendelea kucheza kwa lengo la kubadili matokeo. Kocha hawezi kuwaambia wachezaji wake watoke uwanjani baada ya kuwa wanaongozwa kwa magoli. Badala yake huwaambia waongeze bidii ili na wao wafunge. Kwa nini unaacha mchakato wa kuyapata matokeo baada ya changamoto kukuvuta? Endelea kuweka bidii kuhakikisha unazipita changamoto unazokutana nazo.
Mechi huwa haiahirishwi. Baada ya mechi kuanza, kama hakuna sababu ya msingi ya kuzuia mechi isiendelee, basi mechi huwa haiahirishwi. Una mechi yako hapa duniani, ili uwe salama lazima upate ushindi na ili upate ushindi huna budi kutoiahirisha mechi. Baada ya kuweka mipango yako anza kufanyia, usiiahirishe. Weka nidhamu ya kufanya ulichokipanga bila kujali unajisikia au hujisikii.
Hakuna kukata tamaa mpaka filimbi ya mwisho. Kama filimbi ya mwisho ya mwamuzi haijalia, mchezo unakuwa haujaishi. Wachezaji huendelea kupambana bila kukata tamaa mpaka filimbili ya mwisho hata kupata nafasi ya kubadili matokeo. Kama bado upo hai inamaanisha kuwa bado una nafasi ya kushinda bila kujali magoli uliyokwisha kufungwa na changamoto zako. Unauwezo wa kubadili matokeo ya kushindwa kwako kuwa ushindi usipokata tamaa. Endelea kujifunza na kubadili mbinu ili, hii inongeza nafasi yako ya kushinda.
Ndugu! Una muda maalumu wa kuishi hapa duniani, muda wa mechi yako unazidi kwenda, je unafunga magoli? kama hapana huna budi kubadili mbinu ili uanze kupata mafanikio.
Toa tabia za kushindwa kama kutochukua jukumu la maisha yako, kuahirisha,kutokuwa na malengo, kutoweka akiba nk kisha ingiza tabia za mafanikio kama kuchukua jukumu la maisha yako, kutoahirisha mambo, kuweka akiba nk.
Filimbi ya mwamuzi bado haijalia, fufua mipango uliyoikatia tamaa kisha badili tabia ili kupata ushindi kwenye muda wako uliobaki.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
