Ni Mpaka Umtangulie Huyu Ndipo Utakuwa Mshindi Wa Maisha Yako.
Kwenye mashindano ya magari, gari litakaloibuka mshindi ni lile litakalokuwa limetangulia mengine yote kwenye kituo cha mwisho. Na kama ikitokeo magari yote yamefika kwenye kituo cha mwisho kwa wakati mmoja, basi kutakuwa hakuna mshindi.
Maisha yako hapa duniani ni kama mshindano ya magari. Ili uweze kufanikiwa lazima uwe mbele ya washindani wako. Washindani wa maisha yako ni Ushindani wako na changamoto au vikwazo. Huwezi kushinda na kufanikiwa maisha yanhapa duniani bila ya kuwa mbele ya changamoto.
Ili uwe mshindani lazima uianze safari. Huwezi kusema umeshinda kama hujaianza safari. Safari ya mashindano utaianza pale utakapoweka malengo na kuanza kuyafanyia kazi. Kitendo cha kuanza kuyafanyia kazi ni kuanza mashindano ambayo kama unataka kutimiza malengo yako ni lazima uvishinde vikwazo.
Lazima uwe mbele ya vikwazo. Hakuna safari ya mafanikio isiyo na vikwazo au changamoto. Kadri unavyokuwa na malengo makubwa ya kufanyia kazi ndivyo unavyokuwa kwenye hatari kubwa ya kukutana na changamoto kubwa. Lakini ili uwe mshindi lazima uvishinde vikwazo hivyo bila kujali ukubwa wake.
Uwe mbele ya mitazamo hasi. Moja ya mshindani wako mkubwa wa mashindano yako ni mtazamo hasi. Huwezi kupata ushindi, kama akili yako inaamini kinyume. Huwezi kuchukua hatua kama akili yako inaamini huwezi. Huwezi kuwa tajiri kama akili yako inaamini utajiri ni wa watu fulani tu na wewe si miongoni. Shinda kwa kuwa na mtazamo chanya.
Uwe mbele ya uvivu. Moja ya changamoto ambayo inawazuia watu kutokupiga hatua kubwa ni ukinzani wa mwili. Licha ya kuwa na malengo makubwa ya kufanyia kazi mwili huwa haujitolei kusurubishwa na hivyo kukupa uvivu. Mara ngapi unapanga kufanya kazi kubwa na kwa muda mrefu lakini baada kufanya kazi kwa muda mfupi tu, unahisi umechoka na hujisikii kuendelea? Naamini ni mara nyingi tu! Kuwa mbele ya uvivu huu kwa kuendelea kufanya kazi hata pale unapokuwa hujisikii au kuhisi umechoka. Ukiendelea kuulazimisha, utazoea tu kazi.
Uwe mbele ya tabia ya kuahirisha. Mbona unapanga vizuri sana nini ufanye lakini muda ukifika unasema nitafanya kesho au baadaye! Kuwa mshindi huna budi kuwa mbele ya kikwazo hiki kwa kujenga nidhamu ya kufanya kile ulichopanga. Unaweza ukajenga tabia hii kwa kujipa adhabu baada ya kutotekeleza ulichopanga. Adhabu hiyo inaweza kuwa kutoshiriki kitu unachokipenda sana kam kuangalia mpira au starehe nyingine yoyote. Ukijiwekea adhabu kama hizo zitakusukuma kuchukua hatua ili usikose kushiriki kitu unachokipenda.
Uwe mbele ya kukata tamaa. Safari ya mafanikio huwa ngumu sana. Kuna kushindwa, kuchelewa kupata matokeo, kusemwa nk. Ni rahisi sana kukata tamaa. Unahitaji kuwa mbele ya kikwazo hiki kama unataka kuwa mshindi wa maisha yako. Jenga hamasa ya kudumu ili uweze kuendelea hata pale mambo yanapokuwa magumu. Jenga picha ya matokeo unayotarajia kuyapata mwisho wa safari hiyo ngumu. Yahisi kabisa matokeo hayo. Ukiwa na imani ya kupata matokeo utapata hamasa ya kuendelea ukiamini, ni suala la muda tu kuyapata mafanikio hayo.
Kutangulia hata pua tu. Kwenye mashindano ya mbio za farasi, mshindi huwa ni farasi aliyewatangulia wenzake hata kwa pua tu. Anza kuwa mshindi hata kwa kuwa juu kidogo ya kikwazo chako kisha endelea kuongeza kidogo kidogo mpaka kupata ushindi mkubwa. Kama unataka kushinda kikwazo cha kutoweka akiba kutoka kwenye vipato vyako, anza hatabkwa kuweka hata 5% ya kipato chako. Yaani kwenye sh 10,000/ weka sh 500/ kisha endelea kuongeza kidogo kidogo.
Ndugu! Maisha yako ya mafanikio ni kushinda ndidi ya changamoto au vikwazo vinavyokuwa mbele ya matokeo ya mafanikio. Kazi yako kubwa ni kuhakikisha unakuwa mbele ya vikwazo hivyo ili kutangaza ushindi. Anza kuwa mbele ya vikwazo vilivyoainishwa hapo juu ili kuanza kupata ushindi.
Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz
Tovuti: www.amshauwezo.co.tz
