Hii Ndiyo Njia Ya Kumtafuta Wewe Halisi.


Categories :



Ili mbuzi aweze kufahamika kuwa ni tofauti na kondoo hana budi kutoka nje ya kundi la kondoo na kukaa pembeni. Vinginevyo itakuwa ni vigumu sana yeye kuishi tabia za kimbuzi badala yake ataishia kufuatisha anachokifanya kondoo.

Ili samaki aweze kuogelea na kuendelea kufurahia maisha yake hana budi kutokumuonea wivu wala kuiga jinsi mwewe anavyoweza kuelea angani na kubaki ameganda huko. Kwanza kitendo cha samaki huyo kutoka nje tu ya maji tu kitamsababishia kifo.

Ili mhindi uweze kuota na kustawi hauna budi kutoota chini ya miti mikubwa kwani utasongwa na hata ukikua utashindwa kuzaa. Kumbe ili kila kiumbe kiweze kuonekana na kustawi sana, hakina budi kukaa mazingira fulani huju kikijitenga na vingine.

Na wewe ni kiumbe wa pekee licha ya kuzungukwa na watu wengi. Ili ujijue wewe halisi huna budi kujitenga na watu wengine. Kila aliyoko kwenye kundi hufanana na kundi na hakuna upekee kwenye kundi.

Usifanye kazi yoyote bali yako. Kila mtu halisi ana kazi yake maalumu na siyo kazi yoyote. Unafanikiwa kuwa wewe na kufanya makubwa kwa kufanya kazi yako maalumu yaani uliyoumbwa uifanye. Kazi hiyo maalumu ni kusudi lako. Hii ni sababu ya wewe kuwepo hapa duniani. Kama huishi kusudi lako, basi tambua unamsaidia mtu mwingine kuishi kusudi lake. Hakuna upekee au wewe halisi kwa kufanya chochote.

Usiige bali jiulize kwanza. Jamii au watu wanaokuzunguka wana nguvu ya kukufanya uige maisha yao na kushindwa kuwa wewe. Usiamue kufanya kitu chochote mradi tu kinafanywa na watu wengi. Badala yake kila unapopanga kufanya kitu hasa vile inavyotumia muda mrefu, jiulize je hiki kina uhusiano na kazi yangu maalumu? Kama hapana acha kisha kachague kinachoendana na kazi yako maalumu.

Usiende kokote bali kwako. Samaki akitoka majini na kukaa nchi kavu atakufa tu licha ya uwezo wake mkubwa wa kuogelea. Kadhalika mwewe akizama majini na kuanza kuwinda huko, atakufa licha ya uwezo wake wa kuelea angani. Usipokaa kwenye nafasi yako utakufa, usipokaa kwenye kazi uliyokusudiwa, kazi hiyo itakupa maumivu na kufa hata kiuchumi.

Usimuulize mtu bali moyo wako. Watu wameshindwa kujua wao halisi na kupata mafanikio halisi ya maisha yao kwa kuwauliza watu wengine wao ni nani. Manyu ya wewe ni nani na nini unaweza kufanya ipo ndani yako tu. Hakuna mtu mwingine anayejua vizuri wewe ni nani zaidi yako, hivyo kuwaulize wengine ni kutafuta kudanganywa na kupotezwa. Moyo wako ndiyo unaojua vizuri wewe ni nani. Jiulize ndani yako wewe ni nani ndipo unapata jibu la wewe halisi.

Mafanikio yako halisi yapo kwa wewe halisi. Samaki akiamua kumuiga njiwa kuelea angani badala ya maji atashindwa vibaya na sifa zote za ufundi wake wa kuelea majini zitafutika. Ndivyo ilivyo kwako, huwezi kuyafikia mafanikio makubwa unayostahili kama hutakuwa wewe halisi. Kwa sababu ya wengi kushindwa kutambua wao halisi,wameishia kuwa wa kawaida.

Wakati wako umefika sasa wa kutafuta wewe halisi ili upate mafanikio halisi. Wewe halisi anapatikana ndani yako. Jiulize wewe ni nani? Nini naweza kufanya kwa utofauti mkubwa? Ukishakipata anza kukifanya hicho huku ukijiboresha kufikia ukuu wako.

Imeandikwa na Alfred Mwanyika,
Kocha na Mwalimu(Uwezo Wako Halisi & Mafanikio),
Mawasiliano;
Simu; 0752206899/0714301952
Barua pepe: alfred@amshauwezo.co.tz

Tovuti: www.amshauwezo.co.tz

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *